Kwanini wanawake wana uwezo wa kuona rangi ambazo wengine hawawezi kuziona?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6

Msanii wa uchoraji Conchetta Antico anasema mara alipogundua wanafunzi wake hawakuwa wanaona rangi alizokuwa akiona ilikuwa kama "kumwagiwa maji baridi usoni."

Antico anasema anaona "rangi nyingi" katika matukio ya kila siku, kama vile vivuli, wakati watu wengi wanatambua wigo wa rangi moja pekee.

Alidhani kwamba kila mtu aliuona ulimwengu jinsi alivyouona, hadi alipogundua kutokana na majibu ya wanafunzi wake kwamba haikuwa hivyo.

"Baadaye nilimuuliza mmoja wao, 'Kwa nini hukusema lolote?'" anakumbuka.

"Alijibu, 'Wewe ulikuwa mwalimu. Tulidhani ulikuwa unaonyesha maono yako ya kisanii.'

Antico baadaye aligundua, kupitia uchunguzi wa chembe za urithi, kwamba alikuwa uwezo nadra wa kibiolojia unaofahamika kama Tetrachromacy- uwezo wa hali ya juu wa kuona rangi ambazo wengine hawawezi kuziona.

Aina ya ziada ya seli

Wanadamu wengi wana aina tatu za seli maalumu zinazoitwa "seli za koni" (cones) kwenye utando wa ndani wa jicho (retina).

Kila moja ya seli hizi huitikia masafa mahususi ya urefu wa mawimbi ya mwanga, ambayo kimsingi yanahusiana na rangi nyekundu, kijani, na bluu.

Seli hizi za koni hutuma ishara zake kwenye ubongo. Rangi tunayoiona hutegemea mchanganyiko wa ishara ambazo ubongo hupokea kutoka kwa aina mbalimbali za seli hizo.

Hata hivyo, baadhi ya watu wanaweza pia kuwa na aina ya nne ya seli za koni. Kinadharia, hii ingewezesha ubongo wao kupokea taarifa nyingi zaidi na za aina mbalimbali, jambo ambalo lingeweza kuongeza usikivu kwa rangi katika wigo mzima wa mwanga unaoonekana.

Aina mbili tofauti za jeni

Jeni zinazohusika na kutengeneza seli za koni muhimu kwa rangi nyekundu na kijani ziko kwenye kromosomu ya X. Ili mtu awe na uwezo wa kuona rangi ambazo watu wengine hawazioni, lazima arithi matoleo mawili tofauti ya moja ya jeni hizi na kuziwezesha.

Kwa kuwa wanawake wana kromosomu mbili za X na wanaume kwa kawaida huwa na kromosomu moja ya X, ni wanawake pekee wanaweza kuwa na na uwezo huu wa kibiolojia. Uwepo wa jeni hili kwa wanaume kwa kawaida husababisha aina fulani ya uharibifu wa kuona rangi.

Kuwa na aina ya nne ya seli za koni huitwa "retinal tetrachromacy," na vipimo vya kijenetiki vinaweza kutambua watu ambao wana jeni zinazohitajika kuwa na aina hizi nne za seli.

Kulingana na Mradi wa Quadricolor katika Chuo Kikuu cha Newcastle nchini Uingereza, karibu 12% ya wanawake wanadhaniwa kuwa na uwezo huu wa kijenetiki, ingawa utafiti unaonyesha kuwa idadi hii inaweza kutofautiana miongoni mwa watu.

Hata hivyo, kuwa na seli ya ziada ya koni haimaanishi lazima kuwa na maono makubwa ya rangi.

Hatua hii, inayofahamika kimombo kama "functional tetrachromacy," ni ngumu zaidi kuthibitisha, kulingana na Dkt. Kimberly E. Jameson wa Kituo cha Branson cha Utafiti wa Maono Yaliyotumika katika Chuo Kikuu cha California, Irvine.

Hata hivyo, kuna ushahidi kwamba uwezo huu wa kijenetiki unaweza kusababisha maono yaliyoimarishwa ya rangi.

Mojawapo ya tafiti za Jameson ilionyesha kuwa wanawake wenye aina nne za seli za koni hugawanya wigo wa rangi katika idadi kubwa ya vivuli tofauti, ikidokeza kwamba wanaweza kugundua tofauti ndogo zaidi kati ya rangi kuliko watu wa tetrachroma, ambao wana aina tatu za seli za koni.

Pia kuna ushahidi kutoka kwa ulimwengu wa wanyama. Katika baadhi ya spishi za nyani wa New World, dume wana aina mbili tu za seli za koni zinazogundua rangi, na kwa sababu hiyo maono yao ya rangi ni ya dichromatic, huku jike likiwa na aina tatu za seli za koni na ni za trichromatic.

Wanasayansi wameona kwamba nyani jike hupata na kula matunda mekundu haraka kuliko dume, ikidokeza kwamba labda wanaona rangi hiyo waziwazi na kwa tofauti kubwa zaidi.

Dkt. Jenny Basten, mwanasayansi wa neva wa kuona katika Chuo Kikuu cha Sussex nchini Uingereza, anasema kwamba tukihusisha ugunduzi huu kwa wanadamu wa tetrachromatic, wanawake walio na aina ya nne ya seli za koni wanaweza kuona rangi tofauti na wengine.

Lakini tofauti hii hasa bado ni suala la mjadala na kutokubaliana.

"Rangi zisizoweza kuelezeka"

"Mtazamo mmoja ni kwamba ikiwa mtu ana kipokezi tofauti cha rangi, anaweza kuona rangi ambazo haziwezi kuelezeka, kama vile ambavyo hatuwezi kumwelezea mtu mwenye upofu wa rangi nyekundu na kijani jinsi rangi nyekundu au kijani zinavyoonekana hasa," anasema Dkt. Michael Newall, mwanafalsafa katika Chuo Kikuu cha Adelaide na mwandishi wa makala kuhusu kile ambacho watu wenye uwezo wa kuona rangi nne (tetrachromats) hukiona.

"Lakini kuna uwezekano mwingine," anaendelea, "kwamba watu hawa wanaweza tu kutofautisha tofauti ndogo zaidi kati ya rangi za kawaida."

Kutathmini kisayansi rangi ambazo watu huziona ni kazi ngumu sana.

"Ni vigumui kupima uzoefu wa kibinafsi wa watu kuhusu rangi, hata kwa mtu wa kawaida mwenye uwezo wa kuona rangi tatu za msingi (trichromatic vision)," anasema Basten.

Jameson pia anasema kuwa suala hilo linakuwa tata zaidi tunapozingatia kuwa huenda kuna aina mbalimbali za uwezo wa kuona rangi nne (tetrachromacy), na kwamba kuna tofauti kubwa kati ya watu kulingana na unyeti wa seli ya nne ya jicho inayotambua rangi (cone cell).

Hata hivyo, Basten anasema kuwa kuchunguza uwezo wa watu kutofautisha rangi, au kutathmini jinsi wanavyoona tofauti kati ya aina mbili za rangi, kunaweza kuwasaidia watafiti kuelewa vyema tofauti zilizopo katika jinsi watu wanavyoona rangi.

Unawezaje kumtambua mtu mwenye uwezo wa kuona rangi nyingi zaidi kuliko kawaida?

Utafutaji rahisi mtandaoni utafichua tovuti nyingi zinazodai kutoa kipimo cha kutambua hali ya tetrachromacy (uwezo wa kuona rangi nyingi zaidi kuliko kawaida), lakini wataalamu wanasema haiwezekani kumtambua mtu mwenye hali hiyo kwa njia hii.

Skrini nyingi za kisasa zina njia tatu pekee za rangi—nyekundu, kijani, na bluu. Hivyo, ikiwa watu wenye uwezo wa rangi zaidi kuliko hizi za kawaida bila shaka wanaweza kuona rangi mpya, kuna uwezekano mkubwa rangi hizo hazitaonekana vilevile kwenye skrini.

Newall anasema hali hii inafanya iwe vigumu kupima uwezo huo, lakini ikiwa mtu anatambua mara kwa mara kuwa rangi anazoziona katika ulimwengu halisi ni tofauti na zile anazoziona kwenye skrini, hiyo inaweza kuwa ishara ya tetrachromacy, ingawa jambo hili hutegemea sana teknolojia ya skrini inayotumika.

Kulingana na Jameson, ishara nyingine inayoweza kuonyesha kuwa mtu ana uwezo wa *tetrachromacy* ni hisia zao za mara kwa mara kwamba namna wanavyoona rangi ni tofauti na watu wengine.

"Kwa kawaida, watu hawa hufahamu tangu utotoni kuwa uwezo wao wa kutambua rangi ni sahihi zaidi na muhimu zaidi kuliko ule wa watu wengine," anasema.

Ishara nyingine ya kuvutia ambayo inaweza kuonyesha mtu mwenye uwezo huo ni taa za LED ikilinganishwa na taa za kawaida.

"Wanawake wenye tetracromacy... kwa kawaida hawawezi kuvumilia taa ambazo ni dhaifu katika sehemu ya mawimbi marefu ya mwanga," anasema Jameson.

"Wanaweza kubishana na wenzao wa chumba kimoja na kusema, 'Siwezi kuvumilia mwanga huu. Nachukia taa hizi za fluorescent; zinanifanya nijisikie mgonjwa,'" anaongeza.

Watu ambao baba zao walikuwa na aina ndogo ya ulemavu wa kuona rangi pia wana uwezekano mkubwa wa kuwa tetrachromasia.

Hata hivyo, wataalamu wanasisitiza kwamba ingawa ishara hizi zinaweza kutoa vidokezo, upimaji wa kijenetiki na uchunguzi wa maabara ni viashiria vya kuaminika zaidi.

Kuanzia muundo wa utando wa jicho hadi utendaji wake

Wanasayansi bado hawajui ni kwa nini baadhi ya watu—ambao kibaolojia wana aina nne za seli zinazotambua rangi kwenye utando wa macho yao—wanaweza kutofautisha rangi nyingi zaidi, huku wengine wakiwa hawawezi kufanya hivyo.

"Je, watu hawa wanahitaji kuwa na aina mahususi ya seli za 'cone'? Au ni suala la jinsi walivyojifunza kutumia ishara wanazopata kutoka kwa seli hizi?" anaauliza Basten.

Anadokeza kuwa jambo hili linaweza pia kuhusiana na kiwango cha unyumbufu wa sehemu nyingine za mfumo wa kuona.

"Uwezekano mwingine ni kwamba, ili watu waweze kukuza uwezo wa kutofautisha tofauti hizi za rangi, wanahitaji kutumia ishara hizo za rangi kwa madhumuni ya kivitendo katika maisha yao ya kila siku," anaongeza.

Mchoraji Conchetta Antico anaamini kuwa ndivyo hasa ilivyomtokea yeye.

"Nimejenga uwezo wa kuona rangi," anasema. "Ni kama misuli."

"Nimekuwa nikichora tangu nilipokuwa msichana mdogo... nimetumia takriban saa 100,000 kuchanganya rangi," anaendelea. "Ni jambo ninalolifanya kila siku, karibu wakati wote."