Iran yaishambulia Kuwait, Jordan na Bahrain

Chanzo cha picha, Reuters
Iran imesema imeshambulia vituo vya kijeshi vya Marekani vilivyoko Mashariki ya Kati kwa kutumia ndege zisizo na rubani.
Iran imesema mashambulizi hayo ni ya kulipiza kisasa mashambulizi ya Marekani dhidi ya taifa hilo ambayo yamedumu sasa kwa siku 13 mfululizo.
Awali milipuko iliripotiwa katika maeneo ya pwani ya Ghuba ya Uajemi nchini Iran, pamoja na maeneo ya magharibi, kaskazini na katikati mwa nchi hiyo. Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali ya Iran, watu wanne wameuawa na wengine watano kujeruhiwa katika shambulio lililotokea kusini magharibi mwa taifa hilo.
Kwa kujibu shambulio hilo Iran ilianzisha mashambulizi dhidi ya Kuwait, mshirika wa Marekani, huku ving'ora vya tahadhari vikisikika nchini Bahrain na Jordan. Safari za ndege pia zilisitishwa katika uwanja mkubwa wa ndege nchini Iraq kufuatia taarifa za kuanguka kwa droni karibu na eneo hilo.
Hatua ya Iran imejiri wakati taifa hilo imekuwa ikilaani mpango wa Marekani wa kutumia mali za Iran zilizozuiliwa kufidia uharibifu uliosababishwa na vita, jambo linaloashiria kuongezeka kwa mvutano kati ya mataifa hayo mawili.
Hapo jana, Rais wa Marekani Donald Trump alisema kuwa fidia ya uharibifu uliosababishwa kwa meli za mizigo katika Mlango bahari wa Hormuz italipwa kwa kutumia "fedha za Iran ambazo zinadhibitiwa na Marekani."
"Uharibifu huu unaweza kuwa mkubwa sana, lakini huo ndio utaratibu wa haki na usawa," Trump aliandika kwenye mtandao wake wa Truth Social.
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran, Abbas Araghchi, alijibu kwa kusema kuwa, kunyakua mali za taifa lingine ili kulipia madai yasiyohusiana ni "kuchochea migogoro zaidi."
Soma pia:








