Mahakama yasitisha kwa muda mchakato wa kumuondoa Ramaphosa madarakani

Chanzo cha picha, Getty Images
Mahakama Kuu ya Western Cape nchini Afrika Kusini imempa afueni Rais Cyril Ramaphosa, kwa kusitisha kwa muda mchakato wa kamati ya bunge, ya kumuondoa madarakani.
Mahakama hiyo imesema kesi ya Ramaphosa ya kupinga uhalali wa ripoti iliyobaini kuwa anaweza kuwa na mashtaka ya kujibu kuhusu mwenendo wake, lazima isikilizwe kwanza mwezi Septemba kabla ya mchakato wa kumuondoa madarakni kuendelea.
Kesi hiyo inahusu namna Rais Ramaphosa alivyoshughulikia wizi wa takriban dola 580,000 za Marekani uliotokea mwaka 2020 katika shamba lake la Phala Phala
Jopo la majaji watatu lilisikiliza kesi hiyo. Majaji wawili waliunga mkono ombi la Ramaphosa la kusitisha kwa muda shughuli za kamati ya bunge, huku jaji mmoja akitaka ombi hilo litupiliwe mbali.
Kutokana na uamuzi wa wengi, mchakato wa uchunguzi wa bunge kuhusu uwezekano wa kumuondoa rais huyo madarakani hautaendelea, hadi kesi yake nyingine itakapomalizika.
Ramaphosa amekuwa akikanusha mara kwa mara kufanya kosa lolote na amesisitiza kwamba hatajiuzulu kutokana na sakata hilo maarufu kama ‘Farm Gate’, tangu ilipobainika kuwa alikuwa na kiasi hicho cha fedha za kigeni, ambazo hakuwa ametangaza rasmi, na baadaye zikaibiwa katika shamba lake mwaka wa 2020.
Rais huyo alijitetea kuwa dola 580,000 za Marekani zilizokuwa zimefichwa katika nyumba yake ya kifahari kwenye shamba la Phala Phala, mkoani Limpopo, kaskazini mwa Afrika Kusini, zilikuwa mapato yaliyotokana na mauzo ya nyati.
Soma pia:











