Wakimbizi raia wa DRC wanoishi Burundi wakumbwa na uhaba wa chakula

Chanzo cha picha, Getty Images
Na Robert Kiptoo
BBC Nairobi
Zaidi ya wakimbizi laki moja na thelathini walioko nchini Burundi, wengi wao waliokimbia machafuko na mapigano mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wanakabiliwa na hatari ya ukosefu wa chakula katika miezi ijayo
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, limeonya kuwa linahitaji dola milioni 35 za Marekani ili kuendelea kuwapatia chakula na huduma za lishe wakimbizi hao hadi Agosti mwaka ujao.
WFP imesema kuwa maelfu ya wakimbizi hao wanaoishi katika kambi za muda nchini Burundi kwa sasa wanaishi kwa lishe moja kwa siku huku baadhi wakikosa chakula.
WFP imesema kuwa bila ufadhili mpya, ugawaji wa chakula unaweza kusitishwa kabisa kuanzia mwezi Oktoba mwaka huu.
Wengi wa wakimbizi hao walifika Burundi wakitafuta usalama, mlo wa siku na mahali pa kuishi. Lakini sasa msaada huo ambao umekuwa tegemeo lao kuu uko hatarini kutoweka kabisa.
Tayari upungufu wa fedha umeilazimu shirika hilo la WFP kupunguza mgao wa chakula kwa wakimbizi wengi. Shirika hilo linaonya kuwa ikiwa msaada utasitishwa kabisa, njaa itaongezeka, utapiamlo utakuwa mkubwa zaidi miongoni mwa wakimbizi hao hasa watoto na kina mama.
Mwishoni mwa mwaka uliopita, kuongezeka kwa mapigano mashariki mwa Congo kulisababisha zaidi ya watu laki moja kukimbilia Burundi.
Soma pia:










